Utapeli ni wakati mtu anakudanganya ili akutoe pesa zako. Watapeli wana ujuzi wa kujifanya wao ni wahusika halisi na kwamba wanaweza kukusaidia kwa njia fulani.
Jinsi ya kugundua utapeli
Hapa kuna dalili kuu za utapeli:
- Mawasiliano ambayo hukutarajia - mtu fulani anajitolea kukusaidia na jambo fulani, kama vile akaunti yako ya benki au intaneti, au anapendekeza uwekeze
- Ofa ni nzuri mno kuwa kweli - inaonekana kama mpango wa 'kutajirika haraka', jambo ambalo si la kweli
- Unashinikizwa kufanya jambo haraka - kama vile kuhamisha pesa au kufanya uamuzi wa haraka
Mtapeli anaweza kukuuliza:
- kulipia kitu kwa njia isiyo ya kawaida, kama vile kwa kadi za kupwa kama zawadi
- kusasisha maelezo yako ya kuingia, au umpe manenosiri yako au maelezo mengine ya kibinafsi
- kuthibitisha maelezo yako ya benki ili aweze kukupa 'marudisho ya pesa'
- kumpatia misimbo ya uthibitishaji ya benki
- kubonyeza kiungo (link) anachokutumia
- kupakua programu anazotoa
- kumpa ufikiaji wa mbali kwa kompyuta yako ili 'kurekebisha' shida (ambayo haipo)
Jinsi ya kujikinga na utapeli
ACHA
Ikiwa umewasiliana nawe bila kutarajia, acha na ufikiri kabla ya kujibu.
ANGALIA
Angalia kama mawasiliano anatoka kwa mtu halisi au shirika.
Tafuta nambari yao ya simu iliyoorodheshwa hadharani. Au, ikiwa unamjua mtu huyo, mpigie simu moja kwa moja na uulize ikiwa kweli aliwasiliana nawe.
Angalia mara kwa mara miamala ya kutiliwa shaka kwenye akaunti zako za benki, ripoti ya mikopo na akaunti za ununuzi mtandaoni.
CHUKUA HATUA
Ikiwa unashuku kuwa kuna kitu kibaya, chukua hatua haraka. Zuia au ufute maandishi au barua pepe, au kata simu.
Usitume pesa yoyote. Au, ikiwa umetuma pesa, wasiliana na benki yako au taasisi ya fedha mara moja ili kuripoti utapeli huo.
Onya familia yako na marafiki kuhusu kitu hicho na uangalie 'ofa' zozote za ufuatiliaji ili kurejesha pesa zako zilizopotea.
UELEVU WA PESA (MONEYSMART)
Ili kujilinda dhidi ya watapeli, fuata vidokezo hivi:
- Tumia tovuti zinazoaminika pekee kwa benki, uwekezaji, ununuzi - tafuta ishara ya 'kufuli' katika anwani ya tovuti.
- Usibonyeze viungo (links) katika barua pepe au ujumbe wa maandishi unaotiliwa shaka
- Angalia miamala yako kwa chochote cha kutiliwa shaka
- Tumia manenosiri thabiti na uyabadilishe kila baada ya miezi 6
- Weka maelezo yako ya kibinafsi salama - tarehe ya kuzaliwa, anwani, barua pepe, anwani za mitandao ya kijamii
- Linda kompyuta yako na vifaa vya mkononi - viweke mahali salama nyumbani na utumie programu ya kingavirusi kutoka kwa mtoa huduma anayeaminika
Nini cha kufanya ikiwa umetapeliwa
Iwapo umetapeliwa, fuata hatua hizi ili kuchukua hatua.
- Usitume pesa zaidi. Zuia mawasiliano yote kutoka kwa mtapeli.
- Wasiliana na benki yako au taasisi ya fedha mara moja ili kuripoti utapeli huo. Waambie wasimamishe miamala yoyote.
- Onya familia yako na marafiki kuhusu utapeli huo.
- Jihadharini na utapeli unaowezekana kwa kutumia 'ofa' ili kurejesha pesa zako ikiwa utalipa zaidi.
Ikiwa mtapeli anayo maelezo yako ya kibinafsi, wasiliana na IDCARE kwa 1800 595 160 (Jumatatu hadi Ijumaa, 8am mpaka 5pm). Wanaweza kukusaidia kufanya mpango (bila malipo) ili kupunguza uharibifu.
Kutapeliwa ni tukio la kutisha. Ikiwa unahitaji mtu wa kuzungumza naye (masaa 24 kwa siku, siku 7 kwa wiki) wasiliana na Lifeline kwa 13 11 14 au Beyond Blue kwa 1300 224 636.
Pata usaidizi ikiwa unahitaji
Kuna msaada wa bure unaopatikana, ikiwa unahitaji:
- Kwa usaidizi katika lugha yako, pigia simu kwa huduma ya utafsiri na ukalimani TIS National kwa 131 450. Watapata mkalimani wa kupigia simu huduma unayohitaji usaidizi nayo.
- Kwa usaidizi wa kutatua masuala ya pesa, piga simu bila malipo Nambari ya Msaada ya Deni la Taifa kwa 1800 007 007. Nambari hii ya msaada inafunguliwa Jumatatu hadi Ijumaa, saa 3.30 asubuhi (9:30am) hadi 10.30 jioni (4:30pm).