Kuelewa jinsi aina tofauti za mikopo zinavyofanya kazi. Jua nini cha kufanya kabla ya kukopa pesa, na jinsi ya kudhibiti deni.
Jinsi mikopo inavyofanya kazi
'Mikopo' ni pesa unazokopa kutoka kwa benki au mtoa huduma wa kifedha. Utahitaji kurejesha pesa hizi, pamoja na riba na ada (ikiwa zipo).
'Riba' ni kiasi unacholipa kwa kutumia pesa unazokopa.
'Mkopo' ni pesa unayokopa na kurejesha ndani ya muda uliokubaliwa. Unalipa riba kwa pesa, ambayo inaweza kutobadilika (inabaki sawa) au kubadilika (inaweza kubadilika kwa wakati).
'Deni' ni pesa unazodaiwa, kama vile pesa unazokopa kutoka benki (malipo ya benki au mkopo). Au ununuzi au bili ambayo bado hujalipia.
Ikiwa ungependa kuepuka kutumia mkopo, unaweza kupata 'kadi ya benki isiyo ya mkopo'. Hii hukuruhusu kutumia pesa zako mwenyewe kulipia vitu.
Mikopo na njia zingine za kulipa
Kuna aina tofauti za mikopo na kukopeshwa, kama vile:
- Kadi ya mkopo - inakuwezesha kulipa vitu kwa pesa unazokopa kisha ulipe, kwa kawaida huwa na riba, hadi kikomo kilichoidhinishwa
- Nunua sasa ulipe baadaye - lipia kitu dukani au mtandaoni kwa kiasi kidogo baada ya muda, badala ya kulipa mapema kabisa
- Mkopo wa kibinafsi - mkopo wa muda wa kati kwa kufanya ununuzi mkubwa, kama kununua gari, ambao unalipa na riba
- Mkopo wa nyumba (au rehani) - mkopo wa muda mrefu kutoka kwa benki kununua nyumba au ghorofa, ambayo unalipa pamoja na riba
Unaweza pia kuona 'mikopo ya siku ya malipo' au 'mikopo ya pesa taslimu' ikitangazwa. Ingawa hizi zinaweza kuonekana kama suluhisho la haraka, zinagharimu zaidi katika ada. Kuna njia za bei nafuu za kukopa pesa haraka unapozihitaji, kama vile mikopo isiyo na riba.
Nini cha kufanya kabla ya kukopa
Tambua ni kiasi gani unachoweza kumudu
Kabla ya kupata mkopo, fikiria ni kiasi gani unaweza kumudu kukopa na kurejesha.
Linganisha pesa unazoingia (mshahara wako au 'mapato') na pesa zinazotoka (bili zako au 'gharama').
Kisha tambua malipo yako ya mkopo yatakavyokuwa kiasi gani. Epuka kukopa zaidi ya uwezo wako wa kurejesha.
Linganisha mkopo au mikopo ili kupata ofa bora zaidi
Ikiwa unatafuta friji mpya, haununui ile ya kwanza unayoiona. Utafute friji inayokidhi mahitaji yako kwa bei nzuri zaidi.
Ni sawa unapokopa pesa. Tafuta bidhaa ya mkopo ambayo inakidhi mahitaji yako. Jua nini itagharimu na jinsi ya kulipa kile unachokopa.
Ikiwa kuna jambo huna uhakika nalo, uliza maswali. Au pata usaidizi kutoka kwa familia au marafiki.
Dhibiti mkopo na deni lako
Lipa kwa tarehe ya kukamilisha
Angalia miamala yako ya benki na mikopo mtandaoni, au taarifa zako za kila mwezi.
Tafuta 'tarehe ya kukamilisha' kwenye bili na taarifa zako, na uhakikishe kuwa unalipa mnamo au kabla ya tarehe hiyo.
Lipa kadri uwezavyo kila mwezi
Baadhi ya bidhaa za mkopo, kama vile kadi za mkopo, hukupa kiasi cha 'malipo ya chini' kwenye taarifa yako.
Ikiwa unaweza kufanya malipo ya juu kuliko kiwango cha chini kila mwezi, utalipa deni haraka. Na utaepuka kulipa riba ya ziada au ada za kuchelewa.
Ukilipa tu kwa kiwango cha chini kabisa, utalipa riba zaidi. Inaweza kuchukua muda mrefu kulipa deni lako kikamilifu.
Pata usaidizi ikiwa unahitaji
Kuna msaada wa bure unaopatikana, ikiwa unahitaji:
- Kwa usaidizi katika lugha yako, pigia simu kwa huduma ya utafsiri na ukalimani TIS National kwa 131 450. Watapata mkalimani wa kupigia simu huduma unayohitaji usaidizi nayo.
- Kwa usaidizi wa kutatua masuala ya pesa, piga simu bila malipo Nambari ya Msaada ya Deni la Taifa kwa 1800 007 007. Nambari hii ya msaada inafunguliwa Jumatatu hadi Ijumaa, saa 3.30 asubuhi (9:30am) hadi 10.30 jioni (4:30pm).